1 Abramu akapanda kutoka Misri, yeye, na mkewe, na kila alichokuwa nacho, na Lutu pamoja naye, mpaka kusini.
2 Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu.
3 Akaendelea kusafiri kutoka kusini mpaka Betheli, mahali pale palipokuwapo hema yake kwanza kati ya Betheli na Ai;
4 napo ndipo palipokuwa na madhabahu aliyofanya hapo kwanza; naye Abramu akaliitia jina la BWANA hapo.
5 Na Lutu aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng’ombe na kondoo, na hema.
6 Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja.
7 Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu, na wachunga wanyama wa Lutu; na siku zile Wakanaani na Waperizi walikuwa wakikaa katika nchi.