1 Naye Raheli alipoona ya kuwa hamzalii Yakobo mwana, Raheli alimwonea ndugu yake wivu. Akamwambia Yakobo, Nipe wana; kama sivyo, nitakufa mimi.
2 Yakobo akamghadhibikia Raheli, akasema, Je! Mimi ni badala ya Mungu, aliyekuzuilia uzao wa mimba?
3 Akasema, Yuko mjakazi wangu, Bilha, uingie kwake ili kwamba azae juu ya magoti yangu, nami nipate uzao kwa yeye.
4 Basi akampa Bilha mjakazi wake kuwa mkewe. Yakobo akaingia kwake.