9 Mungu akamtokea Yakobo tena, aliporudi kutoka Padan-aramu akambariki.
10 Mungu akamwambia, Jina lako ni Yakobo; hutaitwa tena Yakobo, lakini Israeli litakuwa jina lako. Akamwita jina lake, Israeli.
11 Mungu akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uzidi ukaongezeke. Taifa na kundi la mataifa watatoka kwako, na wafalme watatoka viunoni mwako.
12 Na nchi hii niliyowapa Ibrahimu na Isaka nitakupa wewe, na uzao wako baada yako nitawapa nchi hiyo.
13 Mungu akakwea juu kutoka kwake mahali hapo aliposema naye.
14 Yakobo akasimamisha nguzo mahali aliposema naye, nguzo ya mawe, akamimina juu yake sadaka ya kinywaji, akamimina mafuta juu yake.
15 Yakobo akapaita mahali pale, Mungu aliposema naye, Betheli.