1 Ikawa, mwisho wa miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto.
2 Na tazama, ng’ombe saba wazuri, wanono, walipanda kutoka mtoni, wakajilisha manyasini.
3 Na tazama, ng’ombe saba wengine wakapanda nyuma yao kutoka mtoni, wabaya, wamekonda, wakasimama karibu na wale ng’ombe wengine ukingoni mwa mto.
4 Kisha hao ng’ombe wabaya waliokonda wakawala wale ng’ombe saba wazuri, wanono. Basi Farao akaamka.
5 Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema.
6 Na tazama, masuke saba membamba, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao.
7 Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu.