3 maji yakadumu kuondoka katika nchi; na mwisho wa siku mia na hamsini maji yakapunguka.
4 Mwezi wa saba, siku ya kumi na saba ya mwezi, safina ikatua juu ya milima ya Ararati.
5 Maji yakapunguka-punguka hata mwezi wa kumi; mwezi huo wa kumi, siku ya kwanza ya mwezi, vilele vya milima vikaonekana.
6 Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya;
7 akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huko na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi.
8 Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi;
9 bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani.