1 Ufunuo juu ya Ninawi. Kitabu cha maono aliyoyaona Nahumu, Mwelkoshi.
2 BWANA ni Mungu mwenye wivu, naye hujilipiza kisasi; BWANA hujilipiza kisasi, naye ni mwingi wa hasira; BWANA hujilipiza kisasi juu ya adui zake, huwawekea adui zake akiba ya hasira.
3 BWANA si mwepesi wa hasira, ana uweza mwingi, wala hatamhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; BWANA ana njia yake katika kisulisuli na tufani, na mawingu ni mavumbi ya miguu yake.
4 Yeye huikemea bahari na kuikausha, pia huikausha mito yote; Bashani hulegea, na Karmeli; hulegea nalo ua la Lebanoni.
5 Milima hutetema mbele zake, navyo vilima huyeyuka; nayo dunia huinuliwa mbele za uso wake, naam, dunia na wote wakaao ndani yake.