13 Tena nikakung’uta nguo yangu, nikasema, Mungu na amkung’ute vivyo hivyo kila mtu nyumbani mwake, na kazini mwake, asiyeitimiza ahadi hiyo; naam, na akung’utwe vivyo hivyo, na kuwa hana kitu. Mkutano wote wakasema, Amina; wakamhimidi BWANA. Nao watu wakafanya kama ahadi hiyo.
14 Tena tangu wakati huo nilipowekwa kuwa liwali wao katika nchi ya Yuda, tangu mwaka wa ishirini hata mwaka wa thelathini na mbili wa Artashasta mfalme, yaani, miaka kumi na miwili, mimi na ndugu zangu hatukula chakula cha liwali.
15 Lakini maliwali wa kwanza walionitangulia, wakawalemea watu, wakawatwalia chakula na mvinyo, zaidi ya shekeli arobaini za fedha; tena watumwa wao nao wakatawala juu ya watu; lakini mimi sikufanya hivyo, kwa kuwa nalimcha Mungu.
16 Naam, hata kazi ya ukuta huu tena nikaishika sana, wala hatukununua mashamba; na watumishi wangu wote wakakusanyika huko kazini.
17 Pamoja na hayo wakawako mezani pangu, katika Wayahudi na mashehe, watu mia na hamsini, zaidi ya wale waliotujia kutoka kwa makafiri waliotuzunguka.
18 Basi, maandalio yaliyoandaliwa kwa siku moja yalikuwa ng’ombe mmoja, na kondoo wazuri sita; tena nikaandaliwa kuku, na mara moja katika siku kumi akiba ya mvinyo ya namna zote; wala kwa hayo yote sikukidai chakula cha liwali, kwa kuwa utumwa ulikuwa mzito juu ya watu hao.
19 Unikumbukie, Ee Mungu wangu, kwa mema, yote niliyowafanyia watu hawa.