1 Basi ikawa, walipoarifiwa Sanbalati, na Tobia, na Geshemu, Mwarabu na adui zetu hao wengine, kwamba nimeujenga ukuta, wala hayakusalia mavunjiko ndani yake; (ijapokuwa hata wakati ule sijaisimamisha milango katika malango);
2 Sanbalati na Geshemu wakatuma wajumbe kwangu, wakasema, Njoo, tukutane huko vijijini katika nchi tambarare ya Ono. Walakini wakakusudi kunifanyia mabaya.
3 Na mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata nisiweze kushuka; mbona kazi ikome, hapo ninapoiacha, niwashukie?
4 Nao wakaniletea maneno kama hayo mara nne; nikawajibu maneno kama yale.
5 Ndipo Sanbalati akamtuma kwangu mtumwa wake vile vile mara ya tano, na barua wazi mkononi mwake;
6 nayo yakaandikwa humo, Habari imeenea katika mataifa, naye Geshemu asema neno lilo hilo, ya kwamba wewe na Wayahudi mwakusudi kuasi; ndiyo sababu waujenga huo ukuta; nawe wataka kuwamiliki, ndivyo wasemavyo.