Omb. 3 SUV

Upendo wa Mungu Huvumilia

1 Mimi ni mtu aliyeona matesoKwa fimbo ya ghadhabu yake.

2 Ameniongoza na kuniendesha katika gizaWala si katika nuru.

3 Hakika juu yangu augeuza mkono wakeMara kwa mara mchana wote.

4 Amechakaza nyama yangu na ngozi yangu;Ameivunja mifupa yangu.

5 Amejenga boma juu yangu,Na kunizungusha uchungu na uchovu.

6 Amenikalisha penye giza,Kama watu waliokufa zamani.

7 Amenizinga pande zote hata siwezi kutoka;Ameufanya mnyororo wangu mzito.

8 Naam, nikilia na kuomba msaada,Huyapinga maombi yangu.

9 Ameziziba njia zangu kwa mawe yaliyochongwa;Ameyapotosha mapito yangu.

10 Alivyo kwangu ni kama dubu aoteaye,Kama simba aliye mafichoni.

11 Amezigeuza njia zangu, na kunirarua-rarua;Amenifanya ukiwa.

12 Ameupinda upinde wake,Na kunifanya niwe shabaha kwa mshale.

13 Amenichoma viunoKwa mishale ya podo lake.

14 Nimekuwa dhihaka kwa watu wangu wote;Wimbo wao mchana kutwa.

15 Amenijaza uchungu,Amenikinaisha kwa pakanga.

16 Amenivunja meno kwa changarawe;Amenifunika majivu.

17 Umeniweka nafsi yangu mbali na amani;Nikasahau kufanikiwa.

18 Nikasema, Nguvu zangu zimepotea,Na tumaini langu kwa BWANA.

19 Kumbuka mateso yangu, na msiba wangu,Pakanga na nyongo.

20 Nafsi yangu ikali ikiyakumbuka hayo,Nayo imeinama ndani yangu.

21 Najikumbusha neno hili,Kwa hiyo nina matumaini.

22 Ni huruma za BWANA kwamba hatuangamii,Kwa kuwa rehema zake hazikomi.

23 Ni mpya kila siku asubuhi;Uaminifu wako ni mkuu.

24 BWANA ndiye fungu langu, husema nafsi yangu,Kwa hiyo nitamtumaini yeye.

25 BWANA ni mwema kwa hao wamngojeao,Kwa hiyo nafsi imtafutayo.

26 Ni vema mtu autarajie wokovu wa BWANANa kumngojea kwa utulivu.

27 Ni vema mwanadamu aichukue niraWakati wa ujana wake.

28 Na akae peke yake na kunyamaza kimya;Kwa sababu Bwana ameweka hayo juu yake.

29 Na atie kinywa chake mavumbini;Ikiwa yamkini liko tumaini.

30 Na amwelekezee yule ampigaye shavu lake;Ashibishwe mashutumu.

31 Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtuHata milele.

32 Maana ajapomhuzunisha atamrehemu,Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake.

33 Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu.Wala kuwahuzunisha.

34 Kuwaseta chini kwa miguuWafungwa wote wa duniani,

35 Kuipotosha hukumu ya mtuMbele zake Aliye juu,

36 Na kumnyima mtu haki yake,Hayo Bwana hayaridhii kabisa.

37 Ni nani asemaye neno nalo likafanyika,Ikiwa Bwana hakuliagiza?

38 Je! Katika kinywa chake Aliye juuHayatoki maovu na mema?

39 Mbona anung’unika mwanadamu aliye haiMtu akiadhibiwa kwa dhambi zake?

40 Na tuchunguze njia zetu na kuzijaribu,Na kumrudia BWANA tena.

41 Na tumwinulie Mungu aliye mbinguniMioyo yetu na mikono.

42 Sisi tumekosa na kuasi;Wewe hukusamehe.

43 Umetufunika kwa hasira na kutufuatia;Umeua, wala hukuona huruma.

44 Umejifunika nafsi yako kwa wingu,Maombi yetu yasipite.

45 Umetufanya kuwa takataka, na vifusiKatikati ya mataifa.

46 Juu yetu adui zetu woteWametupanulia vinywa vyao.

47 Hofu imetujilia na shimo,Ukiwa na uharibifu.

48 Jicho langu lachuruzika mito ya majiKwa ajili ya uvunjifu wa binti ya watu wangu.

49 Jicho langu latoka machozi lisikome,Wala haliachi;

50 Hata BWANA atakapoangaliaNa kutazama toka mbinguni.

51 Jicho langu lanitia huzuni nafsini mwangu,Kwa sababu ya binti zote za mji wangu.

52 Walio adui zangu bila sababuWameniwinda sana kama ndege;

53 Wameukatilia mbali uhai wangu gerezani,Na kutupa jiwe juu yangu.

54 Maji mengi yalipita juu ya kichwa changu,Nikasema, Nimekatiliwa mbali.

55 Naliliitia jina lako, BWANA, kutoka lile shimoLiendalo chini kabisa.

56 Ukaisikia sauti yangu; usifiche sikio lakoIli usisikie pumzi yangu, kwa kilio changu.

57 Ulinikaribia siku ile nilipokulilia;Ukasema, Usiogope.

58 Ee BWANA umenitetea mateto ya nafsi yangu;Umeukomboa uhai wangu.

59 Umekuona kudhulumiwa kwangu, Ee BWANA;Unihukumie neno langu.

60 Umekiona kisasi chao chote,Na mashauri yao yote juu yangu.

61 Ee BWANA, umeyasikia matukano yao,Na mashauri yao yote juu yangu;

62 Midomo yao walioinuka juu yanguNa maazimio yao juu yangu mchana kutwa.

63 Uangalie kuketi kwao, na kuinuka kwao;Wimbo wao ndio mimi.

64 Utawalipa malipo, Ee BWANA,Sawasawa na kazi ya mikono yao.

65 Utawapa ushupavu wa moyo;Laana yako juu yao.

66 Utawafuatia kwa hasira, na kuwaangamizaWasiwe tena chini ya mbingu za BWANA.

Sura

1 2 3 4 5