1 Ee BWANA, kumbuka yaliyotupata;Utazame na kuiona aibu yetu.
2 Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni;Na nyumba zetu kuwa mali ya makafiri.
3 Tumekuwa yatima waliofiwa na baba;Mama zetu wamekuwa kama wajane.
4 Tumekunywa maji yetu kwa fedha;Kuni zetu twauziwa.
5 Watufuatiao wa juu ya shingo zetu;Tumechoka tusipate raha yo yote.
6 Tumewapa hao Wamisri mkono;Na Waashuri nao, ili tushibe chakula.
7 Baba zetu walitenda dhambi hata hawako;Na sisi tumeyachukua maovu yao.
8 Watumwa wanatutawala;Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao.
9 Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu;Kwa sababu ya upanga wa nyikani.
10 Ngozi yetu ni nyeusi kama tanuu;Kwa sababu ya hari ya njaa ituteketezayo.
11 Huwatia jeuri wanawake katika Sayuni;Na mabikira katika miji ya Yuda.
12 Wakuu hutungikwa kwa mikono yao;Nyuso za wazee hazipewi heshima.
13 Vijana huyachukua mawe ya kusagia;Na watoto hujikwaa chini ya kuni.
14 Wazee wameacha kwenda langoni;Na vijana kwenda ngomani.
15 Furaha ya mioyo yetu imekoma;Machezo yetu yamegeuka maombolezo.
16 Taji ya kichwa chetu imeanguka;Ole wetu! Kwa kuwa tumetenda dhambi.
17 Kwa sababu hiyo mioyo yetu imezimia;Kwa ajili ya hayo macho yetu hayaoni vema.
18 Kwa ajili ya mlima Sayuni ulio ukiwa,Mbweha hutembea juu yake.
19 Wewe, BWANA, unadumu milele;Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi.
20 Mbona watusahau sikuzote;Na kutuacha muda huu mwingi?
21 Ee BWANA, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.
22 Isipokuwa wewe umetukataa kabisa;Nawe una hasira nyingi sana juu yetu.