2 Basi na huyu Boazi, je! Siye wa mbari yetu, ambaye ulikuwapo pamoja na wasichana wake? Tazama, usiku wa leo atakuwa akipepeta shayiri pale ugani.
3 Basi wewe oga, ujipake mafuta ujivike mavazi yako, kisha uende kwenye uga; walakini usijionyeshe kwake mtu yule, ila atakapokwisha kula na kunywa.
4 Nayo itakuwa wakati atakapolala, utapaangalia mahali alalapo, nawe uingie, uifunue miguu yake ujilaze hapo; na yeye atakuambia utakalofanya.
5 Akamwambia, Hayo yote unenayo mimi nitayafanya.
6 Basi akashuka mpaka ugani; akafanya yote kama vile mkwewe alivyomwagiza.
7 Ikawa huyo Boazi alipokwisha kula na kunywa, na moyo wake umekunjuka, alikwenda kulala penye mwisho wa chungu ya nafaka; na huyo mwanamke akaja taratibu, akaifunua miguu yake, akajilaza papo hapo.
8 Na ikawa usiku wa manane yule mtu akasituka, akajigeuza; na kumbe! Yupo mwanamke amelala miguuni pake.