8 Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.
9 Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.
10 Ndipo Yoshua akawaamuru maakida wa watu, akisema,
11 Piteni katikati ya matuo, mkawaamuru hao watu, mkisema, Fanyeni tayari vyakula; kwa maana baada ya siku tatu mtavuka mto huu wa Yordani, ili kuingia na kuimiliki nchi awapayo BWANA, Mungu wenu, mpate kuimiliki.
12 Tena Yoshua akawaambia Wareubeni, na Wagadi, na hao wa nusu ya kabila ya Manase, akasema,
13 Likumbukeni neno lile alilowaamuru Musa mtumishi wa BWANA, akisema, BWANA, Mungu wenu, anawapa ninyi raha, naye atawapa nchi hii.
14 Wake zenu, na watoto wenu, na makundi yenu, watakaa katika nchi aliyowapa Musa ng’ambo ya Yordani; bali ninyi mtavuka mbele ya ndugu zenu, hali mmevikwa silaha zenu, watu wote wenye nguvu, na ushujaa, ili mpate kuwasaidia;