Yos. 22 SUV

Makabila ya Mashariki Warudi katika Nchi Zao

1 Wakati huo Yoshua akawaita Wareubeni, na Wagadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase,

2 naye akawaambia, Ninyi mmeyaandama hayo yote mliyoamriwa na Musa, mtumishi wa BWANA, nanyi mmeisikia sauti yangu katika yote niliyowaamuru mimi;

3 hamkuwaacha hao ndugu zenu siku hizi nyingi hata hivi leo, lakini mmeyashika mausia ya amri ya BWANA, Mungu wenu.

4 Na sasa yeye BWANA, Mungu wenu, amewapa ndugu zenu kustarehe, kama alivyowaambia; basi sasa rudini ninyi mwende mahemani kwenu, hata nchi ya milki yenu, ambayo huyo Musa, mtumishi wa BWANA, aliwapa ng’ambo ya pili ya Yordani.

5 Lakini mjibidiishe sana kuzifanya amri na sheria, ambazo Musa, mtumishi wa BWANA, aliwaamuru, kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kwenenda katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na kushikamana na yeye, na kumtumikia kwa moyo wenu wote na nafsi yenu yote.

6 Basi Yoshua akawabarikia, na kuwapa ruhusa waende zao; nao wakaenda mahemani kwao.

7 Basi Musa alikuwa amewapa hiyo nusu moja ya kabila ya Manase urithi katika Bashani; lakini hiyo nusu ya pili Yoshua aliwapa urithi kati ya ndugu zao, ng’ambo ya Yordani upande wa kuelekea magharibi. Zaidi ya hayo Yoshua, hapo alipowapeleka waende zao mahemani kwao, akawabarikia,

8 kisha akanena nao, na kuwaambia, Rudini na mali mengi mahemani kwenu, na ng’ombe wengi sana, na fedha, na dhahabu, na shaba, na chuma, na mavao mengi sana; mzigawanye na ndugu zenu hizo nyara za adui zenu.

9 Basi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase wakarudi, wakatoka kwa wana wa Israeli katika Shilo, ulioko nchi ya Kanaani, ili waende nchi ya Gileadi, hiyo nchi ya milki yao, waliyokuwa wanaimiliki, sawasawa na amri ya BWANA kwa mkono wa Musa.

Madhabahu ya Ukumbusho

10 Nao walipofika pande za Yordani, zilizo katika nchi ya Kanaani, hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na nusu ya kabila ya Manase, wakajenga madhabahu huko karibu na Yordani, iliyoonekana kuwa ni madhabahu kubwa.

11 Wana wa Israeli walisikia ikinenwa, Tazama, wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wamejenga madhabahu huko upande wa mbele wa nchi ya Kanaani, katika nchi iliyo karibu na Yordani, kwa upande huo ulio milki ya wana wa Israeli.

12 Basi, wana wa Israeli waliposikia habari hiyo, mkutano wote wa wana wa Israeli wakakutanika pamoja huko Shilo, ili waende kupigana nao.

13 Kisha wana wa Israeli wakatuma wajumbe waende kwa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, hata nchi ya Gileadi; nao ni hawa, Finehasi mwana wa Eleazari kuhani;

14 na pamoja naye wakuu kumi, mkuu mmoja wa nyumba ya mababa kwa ajili ya kila kabila ya Israeli; nao kila mmoja alikuwa ni kichwa cha nyumba ya mababa katika maelfu ya Israeli.

15 Nao wakawafikilia hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, katika nchi ya Gileadi, na wakasema nao, wakinena,

16 Mkutano wote wa BWANA wanena, Ni kosa gani hili mlilolikosa juu ya Mungu wa Israeli, hata mkakengeuka hivi leo na kuacha kumwandama BWANA, katika kujijengea madhabahu, na kuasi hivi leo juu ya BWANA?

17 Je! Ule uovu wa Peori haututoshi, ambao hamjajitakasa nafsi zenu katika huo hata hivi leo, ijapokuwa ilikuja tauni juu ya mkutano wa BWANA,

18 hata ikawa hamna budi hivi leo kugeuka na kuacha kumwandama BWANA? Kisha itakuwa, kwa kuwa ninyi mwamwasi BWANA hivi leo, kwamba kesho yeye atakasirika na mkutano wote wa Israeli.

19 Basi kwamba hiyo nchi ya milki yenu si tohara, ndipo ninyi vukeni na kuingia nchi ya milki yake BWANA, ambayo maskani ya BWANA inakaa ndani yake, nanyi twaeni milki kati yetu; lakini msimwasi BWANA, wala msituasi sisi, kwa kujijengea madhabahu zaidi ya hiyo madhabahu ya BWANA, Mungu wetu.

20 Je! Huyo Akani mwana wa Zera hakukosa katika vile vitu vilivyowekwa wakfu, na hasira ikauangukia mkutano wote wa Israeli? Kisha mtu huyo hakuangamia peke yake katika uovu wake?

21 Ndipo hapo wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wakajibu, na kuwaambia hao waliokuwa ni vichwa vya maelfu ya Israeli, wakasema,

22 Mungu, Mungu BWANA, naam, Mungu, Mungu BWANA, yeye yuajua, na Israeli naye atajua; kama ni katika uasi, au kama ni katika kosa juu ya BWANA, (usituokoe hivi leo);

23 sisi kujijengea madhabahu ili kukengeuka na kuacha kumwandama BWANA; au kama ni kusongeza juu yake sadaka ya kuteketezwa, au sadaka ya unga, au kama ni kusongeza sadaka za amani juu yake, yeye BWANA mwenyewe na alitake jambo hili;

24 au kama sisi tumefanya jambo hili kwa hadhari sana, tena makusudi, huku tukisema, Katika siku zijazo wana wenu yamkini wakanena na wana wetu, na kusema, Ninyi mna nini na BWANA, yeye Mungu wa Israeli?

25 Kwa kuwa yeye BWANA ameufanya huu mto wa Yordani uwe mpaka katikati ya sisi na ninyi, enyi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, hamna fungu katika BWANA; basi hivyo wana wenu wangewakomesha wana wetu wasimche BWANA.

26 Kwa ajili ya hayo tulisema, Na tufanye tayari ili kujijengea madhabahu, si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, wala kwa sadaka yo yote;

27 bali itakuwa ni ushahidi kati ya sisi na ninyi, tena kati ya vizazi vyetu baada yetu, ili kwamba tufanye huo utumishi wa BWANA mbele yake kwa njia ya sadaka zetu za kuteketezwa, na kwa dhabihu zetu, na kwa sadaka zetu za amani; ili kwamba wana wenu wasiwaambie wana wetu katika zamani zijazo, Ninyi hamna fungu katika BWANA.

28 Kwa hiyo tulisema, Itakuwa, hapo watakapotuambia neno kama hilo, au kuwaambia watu wa vizazi vyetu katika zamani zijazo neno kama hilo, ndipo sisi tutawaambia, Angalieni huu mfano wa madhabahu ya BWANA, walioufanya baba zetu, si kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, wala kwa ajili ya dhabihu; lakini ni ushahidi kati ya sisi na ninyi.

29 Mungu na atuzuie msimwasi BWANA, na kukengeuka hivi leo na kuacha kumwandama BWANA, hata mkajenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, au sadaka za unga, au dhabihu, mbali na ile madhabahu ya BWANA, Mungu wetu, iliyo huko mbele ya maskani yake.

30 Basi Finehasi kuhani, na wakuu wa mkutano, maana, ni hao waliokuwa vichwa vya maelfu ya Israeli waliokuwa pamoja naye, hapo walipoyasikia hayo maneno waliyoyasema hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, maneno hayo yaliwaridhia sana.

31 Naye Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, akawaambia wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, akasema, Siku hii ya leo twajua ya kwamba BWANA yu kati yetu, kwa sababu hamkukosa katika jambo hili mbele ya BWANA; sasa ninyi mmewaokoa wana wa Israeli na mkono wa BWANA.

32 Kisha Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, na hao wakuu, wakarudi na kuwaacha wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, wakatoka katika nchi ya Gileadi, na kuingia nchi ya Kanaani; wakawarudia wana wa Israeli, wakawapa habari.

33 Wana wa Israeli nao wakaliridhia jambo hilo; nao wana wa Israeli wakamhimidi Mungu, wala hawakusema tena habari ya kuwaendea juu yao kupigana nao, wala kuiharibu nchi waliyoikaa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi.

34 Basi hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, wakaiita madhabahu hiyo Edi; wakasema, Kwa kuwa ni ushahidi kati yetu ya kwamba yeye BWANA ndiye Mungu.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24