1 Kisha BWANA akanena na Yoshua, na kumwambia,
2 Nena wewe na wana wa Israeli, uwaambie, Haya, toeni hiyo miji ya makimbilio, ambayo niliwaambia habari zake kwa mkono wa Musa;
3 ili kwamba mwenye kuua mtu, aliyemwua mtu awaye yote pasipo kukusudia, na pasipo kujua, apate kukimbilia kuko; nayo itakuwa ni mahali pa kukimbilia kwenu, kumkimbia huyo ajilipizaye kisasi cha damu.
4 Naye ataikimbilia miji hiyo mmojawapo, naye atasimama hapo penye maingilio ya lango la huo mji, kisha atanena neno lake masikioni mwa wazee wa mji; nao watamtia kwao ndani ya mji, na kumpa mahali, ili apate kukaa kati yao.
5 Na kama huyo mwenye kujilipiza kisasi cha damu akimwandamia, ndipo hawatamtoa huyo mwuaji kumtia mkononi mwake huyo; kwa sababu alimpiga mwenziwe naye hakujua, wala hakumchukia tangu hapo.
6 Naye atakaa katika mji huo, hata hapo atakaposimama mbele ya mkutano kuhukumiwa, hata kifo chake kuhani mkuu mwenye kuwapo siku hizo; ndipo yule mwuaji atarudi, na kuuendea mji wake mwenyewe, na nyumba yake mwenyewe, hata mji huo alioutoka hapo alipokimbia.
7 Nao wakaweka Kedeshi katika Galilaya katika nchi ya vilima ya Naftali, na Shekemu katika nchi ya vilima ya Efraimu, na Kiriath-arba (ndio Hebroni) katika nchi ya vilima ya Yuda.
8 Tena ng’ambo ya pili ya Yordani pande za Yeriko upande wa kuelekea mashariki wakaweka Bezeri ulioko nyikani, katika nchi tambarare ya kabila ya Reubeni, na Ramothi katika Gileadi katika kabila ya Gadi, na Golani katika Bashani katika kabila ya Manase.
9 Miji hiyo ndiyo miji iliyoamriwa kwa ajili ya wana wa Israeli wote, na kwa ajili ya mgeni akaaye kati yao ugenini, ili kwamba mtu awaye yote atakayemwua mtu pasipo kukusudia apate kimbilia huko, asife kwa mkono wa mwenye kujilipiza kisasi cha damu, hata hapo atakapokuwa amekwisha simama mbele ya mkutano.