11 Nayo ikavunjwa siku ile; na hivyo wale kondoo wanyonge walionisikiliza wakajua ya kuwa neno hili ndilo neno la BWANA.
12 Nikawaambia, Mkiona vema, nipeni ujira wangu; kama sivyo, msinipe. Basi wakanipimia vipande thelathini vya fedha, kuwa ndio ujira wangu.
13 Kisha BWANA akaniambia, Mtupie mfinyanzi kima kizuri, hicho nilichotiwa kima na watu hao. Basi nikavitwaa vile vipande thelathini vya fedha, nikamtupia huyo mfinyanzi ndani ya nyumba ya BWANA.
14 Ndipo nikaikata vipande viwili fimbo yangu ya pili, iitwayo Vifungo, ili nipate kuuvunja udugu uliokuwa kati ya Yuda na Israeli.
15 BWANA akaniambia, Jitwalie tena vyombo vya mchungaji mpumbavu.
16 Kwa maana, tazama, mimi nitainua katika nchi hii mchungaji, ambaye hatawaangalia waliopotea, wala hatawatafuta waliotawanyika, wala hatamganga aliyevunjika, wala hatamlisha aliye mzima; bali atakula nyama ya wanono, na kuzirarua-rarua kwato zao.
17 Ole wake mchungaji asiyefaa, aliachaye kundi! Upanga utakuwa juu ya mkono wake, na juu ya jicho lake la kuume; mkono wake utakuwa umekauka kabisa, na jicho lake la kuume litakuwa limepofuka.