Zek. 10 SUV

Matengenezo ya Yuda na Israeli

1 Mwombeni BWANA mvua wakati wa masika, naam, BWANA afanyaye umeme, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi kondeni.

2 Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo waenda zao kama kondoo, wateswa, kwa sababu hapana mchungaji.

3 Hasira yangu imewaka juu ya wachungaji, nami nitawaadhibu mbuzi waume; kwa maana BWANA wa majeshi ameliangalia kundi lake, yaani, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kuwa kama farasi wake mzuri vitani.

4 Kwake yeye litatoka lile jiwe la pembeni, kwake yeye utatoka msumari, kwake yeye utatoka upinde wa vita, kwake yeye atatoka kila mtawala pamoja.

5 Nao watakuwa kama mashujaa, wakanyagao adui zao katika matope ya njia vitani; nao watapiga vita, kwa sababu BWANA yu pamoja nao; na hao wapandao farasi watafadhaishwa.

6 Nami nitaitia nguvu nyumba ya Yuda, nami nitaiokoa nyumba ya Yusufu, nami nitawarudisha, kwa maana nawaonea rehema; nao watakuwa kana kwamba sikuwatupa; kwa maana mimi ni BWANA, Mungu wao, nami nitawasikia.

7 Na watu wa Efraimu watakuwa kama shujaa, na moyo wao utafurahi kana kwamba ni kwa divai; naam, watoto wao wataona mambo haya, na kufurahi; mioyo yao itamfurahia BWANA.

8 Nitawapigia kelele, na kuwakusanya pamoja; kwa maana nimewakomboa; nao wataongezeka kama walivyoongezeka.

9 Nami nitawapanda kama mbegu kati ya mataifa; nao watanikumbuka katika nchi zilizo mbali; nao watakaa pamoja na watoto wao; tena watarudi.

10 Tena nitawarudisha toka nchi ya Misri, nitawakusanya na kuwatoa katika Ashuru; nami nitawaingiza katika nchi ya Gileadi na Lebanoni; ila nafasi ya kuwatosha haitaonekana.

11 Naye atapita kati ya bahari ya mateso, na kuyapiga mawimbi ya bahari, na vilindi vyote vya mto wa Nile vitakauka; na kiburi cha Ashuru kitashushwa; na fimbo ya enzi ya Misri itatoweka.

12 Nami nitawatia nguvu katika BWANA; nao watatembea huko na huko katika jina lake, asema BWANA.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14