1 Ufunuo wa neno la BWANA, lililosemwa juu ya nchi ya Hadraki, na Dameski itakuwa mahali pake pa kustarehe; kwa maana jicho la mwanadamu na la kabila zote za Israeli linamwelekea BWANA;
2 na Hamathi pia iliyo mpakani mwake; na Tiro, na Sidoni, kwa maana ana akili nyingi.
3 Na Tiro alijijengea ngome, akakusanya fedha kama mchanga, dhahabu safi kama matope ya njia kuu.
4 Tazama, Bwana atamwondolea mali zake, naye ataupiga uwezo wake alio nao baharini, naye mwenyewe atateketezwa kwa moto.
5 Ashkeloni ataona haya na kuogopa; Gaza pia, naye atafadhaika sana; na Ekroni, kwa maana taraja lake litatahayarika; na mfalme ataangamia toka Gaza, na Ashkeloni atakuwa hana watu.
6 Na mwana wa haramu atatawala huko Ashdodi, nami nitakatilia mbali kiburi cha Wafilisti.
7 Nami nitaondoa damu yake kinywani mwake, na machukizo yake nitayatoa katika meno yake; yeye naye atakuwa ni mabaki kwa Mungu wetu; naye atakuwa kama mtu mkuu katika Yuda, na Ekroni kama Myebusi.
8 Nami nitapiga kambi yangu pande zote za nyumba yangu ili kuwapinga adui, mtu awaye yote asipite ndani yake wala kurudi; wala mtu aoneaye hatapita tena kati yao; kwa maana sasa nimeona kwa macho yangu.
9 Furahi sana, Ee binti Sayuni;Piga kelele, Ee binti Yerusalemu;Tazama, mfalme wako anakuja kwako;Ni mwenye haki, naye ana wokovu;Ni mnyenyekevu, amepanda punda,Naam, mwana-punda, mtoto wa punda.
10 Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiri mataifa yote habari za amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia.
11 Na kwa habari zako wewe, kwa sababu ya damu ya agano lako, nimewatoa wafungwa wako katika shimo lile lisilo na maji.
12 Irudieni ngome, enyi wafungwa wa tumaini; hata hivi leo nasema ya kwamba nitakurudishia maradufu.
13 Maana nimejipindia Yuda, nimeujaza upinde wangu Efraimu; nami nitawaondokesha wana wako, Ee Sayuni, wapigane na wana wako, Ee Uyunani, nami nitakufanya wewe kuwa kama upanga wa shujaa.
14 Naye BWANA ataonekana juu yao,Na mshale wake utatoka kama umeme;Na Bwana MUNGU ataipiga tarumbeta,Naye atakwenda kwa pepo za kisulisuli za kusini.
15 BWANA wa majeshi atawalinda;Nao watakula na kuyakanyaga mawe ya teo;Nao watakunywa na kufanya kelele kama kwa divai;Nao watajazwa kama mabakuli, kama pembe za madhabahu.
16 Na BWANA, Mungu wao, atawaokoa siku hiyo,Kama kundi la watu wake;Kwa maana watakuwa kama vito vya taji,Vikimeta-meta juu ya nchi yake.
17 Maana wema wake, jinsi ulivyo mwingi!Na uzuri wake, jinsi ulivyo mwingi!Nafaka itawasitawisha vijana wanaume,Na divai mpya vijana wanawake.