1 Tazama, siku moja ya BWANA inakuja, ambayo mateka yatagawanyika kati yako.
2 Kwa maana nitawakusanya mataifa yote walete vita juu ya Yerusalemu; na huo mji utapigwa, nazo nyumba zitatekwa, nao wanawake watatendwa jeuri; na nusu ya watu wa mji watatoka kwenda utumwani; ila mabaki ya watu wa mji hawatakatiliwa mbali.
3 Hapo ndipo atakapotokea BWANA, naye atapigana na mataifa hayo, kama vile alipopigana zamani siku ya vita.
4 Na siku hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima wa Mizeituni, unaoelekea Yerusalemu upande wa mashariki, nao mlima wa Mizeituni utapasuka katikati yake, upande wa mashariki na upande wa magharibi; litakuwako huko bonde kubwa sana; na nusu ya mlima ule utaondoka kwenda upande wa kaskazini, na nusu yake itaondoka kwenda upande wa kusini.
5 Nanyi mtakimbia kwa njia ya bonde la milima yangu; kwa maana bonde lile la milima litaenea hata Aseli; naam, mtakimbia, kama vile mlivyokimbia mbele ya tetemeko la nchi, siku za Uzia, mfalme wa Yuda; na BWANA, Mungu wangu, atakuja, na watakatifu wote pamoja naye.
6 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba nuru yake haitakuwa na mwangaza na kiwi;
7 lakini itakuwa siku moja, iliyojulikana na BWANA; si mchana, wala si usiku; lakini itakuwa, ya kwamba wakati wa jioni kutakuwako nuru.