33 Msidanganyike! Urafiki mbaya huharibu tabia njema.
34 Amkeni! Anzeni kuishi vema, na acheni kutenda dhambi. Baadhi yenu hawamjui Mungu kabisa. Hii nawaambieni, ni aibu kubwa kwenu!
35 Lakini mtu anaweza kuuliza: “Wafu watafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?”
36 Hayo ni maswali ya kijinga! Ukipanda mbegu, isipokufa kwanza haitaota.
37 Unachopanda ni mbegu tu, labda ya ngano au nafaka nyingine, na si mmea mzima ambao hutokea baadaye.
38 Mungu huipa hiyo mbegu mwili anaoutaka mwenyewe; kila mbegu hupata mwili wake wa pekee.
39 Miili ya viumbe vyote si sawa. Miili ya binadamu ni ya namna moja, ya wanyama ni ya namna nyingine, ya ndege ni ya namna nyingine na miili ya samaki pia ni ya namna nyingine.