11 Kwa namna hiyo mtafaulu kupewa haki kamili ya kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
12 Kwa hiyo nitaendelea kuwakumbusheni daima mambo haya, ingawa mmekwisha yafahamu na mko imara katika ukweli mlioupokea.
13 Nadhani ni jambo jema kwangu, muda wote niishio hapa duniani, kuwapeni moyo na kuwakumbusheni juu ya mambo haya.
14 Najua kwamba karibu nitauweka kando mwili huu wenye kufa, kama Bwana alivyoniambia waziwazi.
15 Basi, nitajitahidi kusudi baada ya kufariki kwangu mweze kuyakumbuka mambo haya kila wakati.
16 Wakati tulipowafundisheni juu ya ukuu wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, hatukutegemea hadithi tupu zisizo na msingi. Sisi tuliuona utukufu wake kwa macho yetu wenyewe.
17 Sisi tulikuwapo wakati alipopewa heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba, wakati sauti ilipomjia kutoka kwake yeye aliye Utukufu Mkuu, ikisema: “Huyu ni Mwanangu mpenzi ambaye nimependezwa naye.”