14 Basi, wakumbushe watu wako mambo haya na kuwaonya mbele ya Mungu waache ubishi juu ya maneno. Ubishi huo haufai, ila huleta tu uharibifu mkuu kwa wale wanaousikia.
15 Jitahidi kupata kibali kamili mbele ya Mungu kama mfanyakazi ambaye haoni haya juu ya kazi yake na ambaye hufundisha sawa ule ujumbe wa kweli.
16 Jiepushe na majadiliano yasiyofaa na ya kipumbavu; kwani hayo huzidi kuwatenga watu mbali na Mungu.
17 Mafundisho ya aina hiyo ni kama donda linalokula mwili. Miongoni mwa hao waliofundisha hayo ni Humenayo na Fileto.
18 Hawa wamepotoka kabisa mbali na ukweli, na wanatia imani ya watu wengine katika wasiwasi kwa kusema ati ufufuo wetu umekwisha fanyika.
19 Lakini msingi thabiti uliowekwa na Mungu uko imara, na juu yake yameandikwa maneno haya: “Bwana anawafahamu wale walio wake,” na “Kila asemaye yeye ni wa Bwana, ni lazima aachane na uovu.”
20 Katika nyumba kubwa kuna mabakuli na vyombo vya kila namna: Vingine ni vya fedha na dhahabu, vingine vya mbao na udongo, vingine vya matumizi ya heshima na vingine kwa ajili ya matumizi ya kawaida.