35 “Muwe tayari mmejifunga mkanda kiunoni, na taa zenu ziwe zinawaka;
36 muwe kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka harusini, ili wamfungulie mara atakapobisha.
37 Heri yao watumishi wale ambao bwana wao atakaporudi atawakuta wanakesha! Nawaambieni hakika, huyo bwana atajifunga mkanda kiunoni, atawaketisha mezani na kuwahudumia.
38 Hata kama atarudi usiku wa manane au alfajiri na kuwakuta wanakesha, heri yao watumishi hao!
39 Jueni kwamba, kama mwenye nyumba angejua saa ambayo mwizi atakuja, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe.
40 Nanyi, kadhalika muwe tayari, maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia.”
41 Petro akamwambia, “Bwana, mfano huo ni kwa ajili yetu tu, au ni kwa ajili ya watu wote?”