33 Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio:
34 “Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu!”
35 Yesu akamkemea huyo pepo akisema: “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!” Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo.
36 Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, “Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!”
37 Habari za Yesu zikaenea mahali pote katika eneo lile.
38 Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye.
39 Yesu akaja akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Yule mama akainuka mara, akawatumikia.