22 Basi, Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohane yale mliyojionea na kuyasikia: Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari Njema.
23 Heri mtu yule ambaye hana mashaka nami!”
24 Hapo wajumbe wa Yohane walipokwisha kwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu juu ya Yohane: “Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo?
25 Basi, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevaa mavazi maridadi? Wanaovaa mavazi maridadi na kuishi maisha ya anasa, hukaa katika majumba ya wafalme!
26 Basi, niambieni, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii.
27 Huyu Yohane ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu:‘Tazama mimi namtuma mtumishi wangu akutangulie;ambaye atakutayarishia njia yako.’”
28 Yesu akamalizia kwa kusema, “Nawaambieni, kati ya binadamu wote hakuna aliye mkubwa zaidi kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa Mungu ni mkubwa kuliko yeye.”