24 Siku ya pili yake walifika Kaisarea na huko Kornelio alikuwa anawangojea pamoja na jamaa na marafiki aliokuwa amewaalika.
25 Petro alipokuwa anaingia, Kornelio alitoka nje kumlaki, akapiga magoti mbele yake na kuinama chini kabisa.
26 Lakini Petro alimwinua, akamwambia, “Simama, kwa maana mimi ni binadamu tu.”
27 Petro aliendelea kuongea na Kornelio wakiwa wanaingia nyumbani ambamo aliwakuta watu wengi wamekusanyika.
28 Petro akawaambia, “Nyinyi wenyewe mnajua kwamba Myahudi yeyote amekatazwa na sheria yake ya dini kushirikiana na watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amenijulisha nisimfikirie mtu yeyote kuwa najisi au mchafu.
29 Kwa sababu hiyo, mliponiita nimekuja bila kusita. Basi, nawaulizeni: Kwa nini mmeniita?”
30 Kornelio akasema, “Siku tatu zilizopita saa kama hii, saa tisa alasiri, nilikuwa nikisali chumbani mwangu. Ghafla, mtu aliyekuwa amevaa mavazi yenye kungaa alisimama mbele yangu,