1 Basi, watu wengine walifika Antiokia kutoka Yudea wakaanza kuwafundisha wale ndugu wakisema, “Kama hamtatahiriwa kufuatana na mapokeo kama alivyoamuru Mose, hamtaweza kuokolewa.”
2 Jambo hili lilisababisha ubishi mkubwa, na baada ya Paulo na Barnaba kujadiliana nao, ikaamuliwa Paulo na Barnaba pamoja na waumini kadhaa wa lile kanisa la Antiokia waende Yerusalemu kuwaona wale mitume na wazee kuhusu jambo hilo.
3 Basi, kanisa liliwaaga, nao walipokuwa wanapitia Foinike na Samaria waliwaeleza watu jinsi mataifa mengine yalivyomgeukia Mungu. Habari hizo zikawafurahisha sana ndugu hao wote.
4 Walipofika Yerusalemu walikaribishwa na kanisa, mitume na wazee; nao wakawapa taarifa juu ya yote Mungu aliyoyafanya pamoja nao.
5 Lakini waumini wengine waliokuwa wa kikundi cha Mafarisayo walisimama, wakasema, “Ni lazima watu wa mataifa mengine watahiriwe na kufundishwa kuifuata sheria.”