15 Baada ya huyo mama pamoja na jamaa yake kubatizwa, alitualika akisema, “Kama kweli mmeona kwamba mimi namwamini Bwana, karibuni nyumbani kwangu mkakae.” Akatuhimiza twende.
16 Siku moja, tulipokuwa tunakwenda mahali pa kusali, msichana mmoja aliyekuwa na pepo mwenye uwezo wa kuagua alikutana nasi. Msichana huyo alikuwa anawapatia matajiri wake fedha nyingi kwa uaguzi wake.
17 Basi, huyo msichana alimfuata Paulo na sisi, akipiga kelele na kusema, “Hawa watu ni watumishi wa Mungu Mkuu. Wanawatangazieni njia ya wokovu.”
18 Akawa anafanya hivyo kwa siku nyingi hata siku moja Paulo alikasirika, akamgeukia na kumwambia huyo pepo, “Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu!” Mara huyo pepo akamtoka.
19 Matajiri wa yule msichana walipoona kwamba tumaini lao la kupata mali limekwisha, waliwakamata Paulo na Sila, wakawaburuta mpaka hadharani, mbele ya wakuu.
20 Wakawashtaki kwa mahakimu wakisema, “Watu hawa ni Wayahudi na wanafanya fujo katika mji wetu.
21 Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Roma haturuhusiwi kuzikubali wala kuzifuata.”