29 Yule kijana akamwambia, ‘Sitaki!’ Lakini baadaye akabadili nia, akaenda kufanya kazi.
30 Yule baba akamwambia mtoto wake wa pili vivyo hivyo, naye akamjibu, ‘Naam baba!’ Lakini hakuenda kazini.
31 Je, ni nani kati ya hawa wawili aliyetimiza matakwa ya baba yake?” Wakamjibu, “Yule mtoto wa kwanza.”Basi, Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, watozaushuru na waasherati wataingia katika ufalme wa Mungu kabla yenu.
32 Maana Yohane alikuja kwenu akawaonesha njia adili ya kuishi, nanyi hamkumwamini; lakini watozaushuru na waasherati walimwamini. Hata baada ya kuona hayo yote nyinyi hamkutubu na kumsadiki.”
33 Yesu akasema, “Sikilizeni mfano mwingine. Mtu mmoja mwenye nyumba alilima shamba la mizabibu; akalizungushia ukuta, akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga humo mnara pia. Kisha akalikodisha kwa wakulima, akasafiri kwenda hadi nchi ya mbali.
34 Wakati wa mavuno ulipofika, aliwatuma watumishi wake kwa wale wakulima, ili wakachukue sehemu ya mavuno yake.
35 Wale wakulima wakawakamata hao watumishi; mmoja wakampiga, mwingine wakamuua na mwingine wakampiga mawe.