19 Yesu akaondoka pamoja na wanafunzi wake, akamfuata.
20 Mama mmoja, mgonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, alimfuata Yesu nyuma, akagusa pindo la vazi lake.
21 Alifanya hivyo kwani alifikiri moyoni: “Nikigusa tu vazi lake, nitapona.”
22 Basi, Yesu akageuka akamwona, akamwambia, “Binti, jipe moyo! Imani yako imekuponya.” Mama huyo akapona saa ileile.
23 Kisha Yesu akaingia nyumbani kwa yule ofisa. Na alipowaona wapiga filimbi na umati wa watu wanaoomboleza,
24 akasema, “Ondokeni hapa! Msichana huyu hakufa, amelala tu.” Nao wakamcheka.
25 Basi, umati wa watu ulipoondolewa, Yesu aliingia ndani, akamshika huyo msichana mkono, naye akasimama.