1 Kisha nikaona mnyama mmoja akitoka baharini. Alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na kila pembe ilikuwa na taji. Jina la kashfa lilikuwa limeandikwa juu ya vichwa hivyo.
2 Mnyama huyo niliyemwona alikuwa kama chui; miguu yake kama ya dubu na kinywa chake kama cha simba. Lile joka likampa huyo mnyama nguvu yake, kiti chake cha enzi na uwezo mkuu.
3 Kichwa kimojawapo cha huyo mnyama kilionekana kama kilikwisha jeruhiwa vibaya sana, lakini jeraha hilo lilikuwa limepona. Dunia nzima ilishangazwa na huyo mnyama na kumfuata.
4 Watu wote wakaliabudu lile joka kwa sababu lilimpa huyo mnyama uwezo wake. Wakamwabudu pia huyo mnyama wakisema, “Nani aliye kama huyu mnyama? Ni nani awezaye kupigana naye?”
5 Kisha huyo mnyama akaruhusiwa kusema maneno ya kujigamba na kumkufuru Mungu; akaruhusiwa kuwa na mamlaka kwa muda wa miezi arubaini na miwili.
6 Basi, akaanza kumtukana Mungu, kulitukana jina lake, makao yake, na wote wakaao mbinguni.