8 Malaika wa pili alimfuata huyo wa kwanza akisema, “Ameanguka! Naam, Babuloni mkuu ameanguka! Babuloni ambaye aliwapa mataifa yote wainywe divai yake – divai kali ya uzinzi wake!”
9 Na malaika wa tatu aliwafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Yeyote anayemwabudu yule mnyama na sanamu yake na kukubali kutiwa alama yake juu ya paji la uso wake au juu ya mkono wake,
10 yeye mwenyewe atakunywa divai ya ghadhabu ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake bila kuchanganywa na maji. Mtu huyo atateseka ndani ya moto wa madini ya kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele ya Mwanakondoo.
11 Moshi wa moto unaowatesa hupanda juu milele na milele. Watu hao waliomwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa alama ya jina lake, hawatakuwa na nafuu yoyote usiku na mchana.”
12 Hivyo, ni lazima watu wa Mungu, yaani wale wanaotii amri za Mungu na kumwamini Yesu, wawe na uvumilivu.
13 Kisha, nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika! Heri watu ambao tangu sasa wanakufa wakiwa wameungana na Bwana.” Naye Roho asema, “Naam! Watapumzika kutoka taabu zao; maana matunda ya jasho lao yatawafuata.”
14 Kisha, nikatazama, na kumbe palikuwapo wingu jeupe hapo. Na juu ya wingu hilo alikuwako aliye kama Mwana wa Mtu. Alikuwa amevaa taji ya dhahabu kichwani, na kushika mundu mkali mkononi mwake.