12 Macho yake ni kama mwali wa moto, na alikuwa amevaa taji nyingi kichwani. Alikuwa ameandikwa jina ambalo hakuna mtu alijuaye isipokuwa tu yeye mwenyewe.
13 Alikuwa amevaa vazi lililokuwa limelowekwa katika damu. Na jina lake huyo ni “Neno la Mungu”.
14 Majeshi ya mbinguni yalimfuata yakiwa yamepanda farasi weupe na yamevaa mavazi ya kitani, meupe na safi.
15 Upanga mkali hutoka kinywani mwake, na kwa upanga huo atawashinda watu wa mataifa. Yeye ndiye atakayetawala kwa fimbo ya chuma na kuikamua divai katika chombo cha kukamulia zabibu za ghadhabu kuu ya Mungu Mwenye Nguvu.
16 Juu ya vazi lake, na juu ya paja lake, alikuwa ameandikwa jina: “Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.”
17 Kisha, nikamwona malaika mmoja amesimama katika jua. Akapaza sauti na kuwaambia ndege wote waliokuwa wanaruka juu angani, “Njoni! Kusanyikeni pamoja kwa karamu kuu ya Mungu.
18 Njoni mkaitafune miili ya wafalme, ya majemadari, ya watu wenye nguvu, ya farasi na wapandafarasi wao; njoni mkaitafune miili ya watu wote: Walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.”