1 Kila kuhani mkuu ambaye huchaguliwa miongoni mwa watu hupewa jukumu la kushughulikia mambo ya Mungu kwa niaba ya watu, kutolea zawadi na tambiko kwa ajili ya dhambi.
2 Maadamu yeye mwenyewe ni dhaifu, anaweza kuwatendea kwa huruma wale wasiojua kitu na wanaofanya makosa.
3 Kwa sababu hiyo anapaswa kutoa tambiko si tu kwa ajili ya watu, bali pia kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.
4 Hakuna mtu awezaye kujifanya mwenyewe kuwa kuhani mkuu. Kila mmoja huteuliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kama alivyokuwa Aroni.