3 Mimi nilijulishwa kwa njia ya ufunuo mpango wake uliofichika. (Nimeandika kwa ufupi juu ya jambo hili,
4 nanyi mkiyasoma maneno yangu mtaweza kujua jinsi ninavyoielewa siri hiyo ya Kristo).
5 Zamani watu hawakujulishwa siri hiyo; lakini sasa Mungu amewajulisha mitume na manabii wake watakatifu kwa njia ya Roho.
6 Siri yenyewe ni hii: Kwa njia ya Injili watu wa mataifa mengine wanapata sehemu yao pamoja na Wayahudi katika zile baraka za Mungu; wao ni viungo vya mwili uleule, na wanashiriki ahadi ileile aliyofanya Mungu kwa njia ya Kristo Yesu.
7 Mimi nimefanywa kuwa mtumishi wa Injili kwa neema ya pekee aliyonijalia Mungu kwa uwezo wake mkuu.
8 Mimi ni mdogo kuliko watu wote wa Mungu; lakini amenijalia neema yake, ili niwahubirie watu wa mataifa utajiri wake Kristo usiopimika;
9 tena niwaangazie watu wote waone jinsi mpango wa Mungu uliofichika unavyotekelezwa. Mungu aliye Muumba wa vitu vyote alificha hiyo siri yake tangu milele,