21 Alipokwisha sema hayo, Yesu alifadhaika sana rohoni, akasema wazi, “Kweli nawaambieni, mmoja wenu atanisaliti!”
22 Wanafunzi wakatazamana wasiweze kabisa kujua anamsema nani.
23 Mmoja wa wanafunzi, ambaye Yesu alikuwa anampenda sana, alikuwa ameketi karibu na Yesu.
24 Basi, Simoni Petro akamwashiria na kusema: “Mwulize anasema juu ya nani.”
25 Mwanafunzi huyo akasogea karibu zaidi na Yesu, akamwuliza, “Bwana, ni nani?”
26 Yesu akajibu, “Yule nitakayempa kipande cha mkate nilichochovya katika sahani, ndiye.” Basi, akatwaa kipande cha mkate, akakichovya katika sahani, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti.
27 Yuda alipokwisha pokea kipande hicho, Shetani akamwingia. Basi Yesu akamwambia, “Unachotaka kufanya, kifanye haraka!”