2 Siku moja Nikodemo alimwendea Yesu usiku, akamwambia, “Rabi, tunajua kwamba wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, maana hakuna mtu awezaye kufanya ishara unazozifanya Mungu asipokuwa pamoja naye.”
3 Yesu akamwambia, “Kweli nakuambia, mtu asipozaliwa tena hataweza kuuona ufalme wa Mungu.”
4 Nikodemo akamwuliza, “Mtu mzima awezaje kuzaliwa tena? Hawezi kuingia tumboni mwa mama yake na kuzaliwa tena!”
5 Yesu akamjibu, “Kweli nakuambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu.
6 Mtu huzaliwa kimwili kwa baba na mama, lakini huzaliwa kiroho kwa Roho.
7 Usistaajabu kwamba nimekuambia kuwa ni lazima kuzaliwa upya.
8 Upepo huvuma kuelekea upendako; waisikia sauti yake, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda. Ndivyo ilivyo kwa mtu aliyezaliwa kwa Roho.”