16 Hapo Yesu akawajibu, “Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma.
17 Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe.
18 Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake mwenyewe; lakini anayetafuta sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na ndani yake hamna uovu wowote.
19 Je, Mose hakuwapeni sheria? Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishika sheria. Kwa nini mnataka kuniua?”
20 Hapo watu wakamjibu, “Una pepo wewe! Nani anataka kukuua?”
21 Yesu akawajibu, “Kuna jambo moja nililofanya, nanyi mnalistaajabia.
22 Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri. (Si kwamba desturi hiyo ilitoka kwa Mose, bali ilitoka kwa mababu). Sasa nyinyi humtahiri mtu hata siku ya Sabato.