6 Solomoni akamwambia, “Ulimwonesha mtumishi wako Daudi, baba yangu, fadhili nyingi, kwa sababu alikutumikia kwa uaminifu, uadilifu na kwa haki; na umedumisha fadhili zako kwa kumpa mwana anayeketi sasa kwenye kiti chake cha enzi.
7 Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, umeniweka mimi mtumishi wako kuwa mfalme mahali pa baba yangu Daudi, ijapokuwa ningali mtoto mdogo na sijui namna ya kutekeleza wajibu huu.
8 Na hapa umeniweka kati ya watu wako ambao umewachagua; nao ni wengi hata hawawezi kuhesabika kwa wingi wao.
9 Kwa hiyo, nakuomba unipe mimi mtumishi wako moyo wa kusikia ili kuamua watu wako, niweze kutambua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuhukumu watu wako walio wengi hivi?”
10 Ombi hili la Solomoni lilimfurahisha Mwenyezi-Mungu,
11 naye akamwambia, “Kwa kuwa umetoa ombi hili, na hukujiombea maisha marefu au mali, na wala hukuomba adui zako waangamizwe, bali umejiombea utambuzi wa kutoa hukumu au kutenda haki
12 basi, sasa nakutimizia kama ulivyoomba. Tazama, nakupa hekima na akili kiasi ambacho hapana mtu mwingine aliyepata kuwa nacho kabla yako, na wala hatatokea mwingine kama wewe baada yako.