8 Solomoni akamwambia Mungu, “Ulimwonesha baba yangu Daudi fadhili nyingi, na umenijalia kuwa mfalme mahali pake.
9 Sasa, ee Mungu, Mwenyezi-Mungu, itimize ahadi uliyompa baba yangu Daudi. Umenitawaza niwe mfalme juu ya watu hawa walio wengi kama mavumbi.
10 Kwa hiyo, nakuomba unipe hekima na maarifa ili niweze kuwatawala watu wako vizuri. La sivyo, nitawezaje kuwatawala hawa watu wako walio wengi hivi?”
11 Mungu akamjibu Solomoni, “Kwa kuwa jambo hili uliloomba limo moyoni mwako, na wala hukuomba mali, wala utajiri, wala heshima wala hukuomba wanaokuchukia waangamizwe, wala maisha marefu, lakini umeomba hekima na maarifa ili uwatawale vizuri watu wangu ambao nimekupa uwe mfalme wao,
12 ninakupa hekima na maarifa. Pia, nitakupa utajiri, mali na heshima zaidi ya mfalme mwingine yeyote aliyekuwako kabla yako na mfalme mwingine yeyote atakayetawala baada yako.”
13 Basi, Solomoni aliondoka mahali hapo pa kuabudia, huko Gibeoni, lilipokuwa hema la mkutano, akarudi Yerusalemu. Akaitawala Israeli.
14 Solomoni alikusanya magari ya farasi na wapandafarasi; alikuwa na magari ya farasi 1,400, na wapandafarasi 12,000, ambao aliwaweka katika miji yenye vituo vya magari ya farasi na kwake katika Yerusalemu.