18 Rehoboamu alioa mke, jina lake Mahalathi binti Yeremothi mwana wa Daudi. Mama yake alikuwa Abihaili binti Eliabu, mwana wa Yese.
19 Naye alimzalia wana watatu: Yeushi, Shemaria na Zahamu.
20 Baadaye, alimwoa Maaka binti Absalomu, naye akamzalia Abiya, Atai, Ziza na Shelomithi.
21 Rehoboamu alioa wake kumi na wanane na masuria sitini, akazaa watoto wa kiume ishirini na wanne na mabinti sitini. Miongoni mwa wake zake wote na masuria wake, alimpenda Maaka binti Absalomu zaidi.
22 Hivyo akamchagua Abiya, mwana wa Maaka, awe mkuu kati ya ndugu zake, kwani alinuia kumfanya awe mfalme.
23 Rehoboamu alifanya jambo la busara, akawatawanya baadhi ya wanawe katika nchi yote ya Yuda na Benyamini akiwaweka katika miji yote yenye ngome. Wakiwa humo, aliwapa vyakula tele na pia akawaoza wake wengi.