1 Abiya alianza kutawala Yuda mnamo mwaka wa kumi na nane wa utawala wa mfalme Yeroboamu.
2 Alitawala kwa muda wa miaka mitatu akiwa Yerusalemu. Mama yake alikuwa Maaka binti Urieli wa Gibea.Kulitokea vita kati ya Abiya na Yeroboamu.
3 Abiya alijiandaa kupigana vita akiwa na jeshi la askari hodari 400,000, naye Yeroboamu akamkabili na jeshi lake la askari hodari 800,000.
4 Mfalme Abiya alisimama juu ya mlima Semaraimu, ulioko kati ya milima ya Efraimu, akamwambia Yeroboamu na watu wa Israeli, “Nisikilize ewe Yeroboamu na watu wote wa Israeli!
5 Je, hamjui kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, alimwahidi Daudi kwa kufanya naye agano lisilovunjika kuwa daima, wafalme wote wa Israeli watatoka katika uzao wake?
6 Lakini Yeroboamu mwana wa Nebati mtumishi wa Solomoni, mwana wa Daudi alimwasi bwana wake.
7 Baadaye, alijikusanyia kikundi cha mabaradhuli, watu wapumbavu wasiofaa kitu, nao wakamshawishi Rehoboamu mwana wa Solomoni, kutenda yale waliyotaka wao, naye hangeweza kuwazuia kwani wakati huo alikuwa bado kijana bila uzoefu mwingi.