1 Mwishowe, Abiya alifariki na kuzikwa katika mji wa Daudi na Asa mwanawe akatawala mahali pake. Wakati wa Asa, kulikuwa na amani nchini kwa muda wa miaka kumi.
2 Asa alitenda yaliyokuwa mazuri na mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake.
3 Aliondoa nchini madhabahu za kigeni na mahali pa kuabudia miungu mingine, akabomoa minara na kuzikatakata sanamu za Ashera.
4 Aliwaamuru watu wa Yuda wamtafute Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, na kuzitii sheria na amri.
5 Pia aliondoa mahali pote pa kuabudia miungu mingine na meza za kufukizia ubani kutoka katika miji yote ya Yuda; halafu ufalme wake ulikuwa na amani chini ya utawala wake.
6 Alijenga miji yenye ngome katika Yuda wakati huo wa amani, na kwa muda wa miaka kadhaa, hapakutokea vita kwa maana Mwenyezi-Mungu alimpa amani.
7 Naye akawaambia watu wa Yuda, “Na tuiimarishe miji kwa kuizungushia kuta na minara na malango yenye makomeo. Nchi bado imo mikononi mwetu kwa maana tumeyatenda mapenzi yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, naye ametupa amani pande zote.” Basi wakajenga, wakafanikiwa.