14 Walimwapia Mwenyezi-Mungu kwa sauti kuu, wakapaza sauti zaidi, wakapiga tarumbeta na baragumu.
15 Watu wote wa Yuda walikuwa na furaha tele kwa kuwa walikuwa wameapa kwa moyo wote. Walikuwa wamemtafuta kwa dhati, wakampata. Naye Mwenyezi-Mungu akawapa amani pande zote.
16 Mfalme Asa alimwondoa hata Maaka, mama yake, katika cheo chake cha mama malkia, kwa sababu alitengeneza sanamu ya kuchukiza ya Ashera, mungu wa kike. Asa alikatilia mbali sanamu hiyo, akaipondaponda na kuiteketeza katika bonde la kijito Kidroni.
17 Lakini hata hivyo mahali pa kutambikia miungu mingine katika Israeli hapakuharibiwa; lakini yeye alikuwa na moyo mwaminifu maisha yake yote.
18 Alivirudisha katika nyumba ya Mungu vifaa vyote vilivyowekwa wakfu na baba yake pamoja na vile alivyoviweka wakfu yeye mwenyewe: Fedha na dhahabu na vyombo vinginevyo.
19 Hapakuwa na vita tena nchini mpaka mwaka wa thelathini na tano wa utawala wake Asa.