9 Asa aliwaita watu wote wa Yuda na Benyamini, na wengine wote waliokuwa wakikaa nchini mwake kutoka Efraimu, Manase na Simeoni. Hawa walikuja kwake walipoona kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, alikuwa pamoja naye.
10 Wote walikusanyika Yerusalemu katika mwezi wa tatu wa mwaka wa kumi na tano wa utawala wake Asa.
11 Siku hiyo, walimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za ng'ombe 700 na kondoo 7,000, kutoka katika zile nyara walizoteka.
12 Hapo wakafanya agano, ya kuwa watamtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, kwa moyo wote na kwa roho yao yote;
13 na kwamba yeyote asiyemtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, awe kijana au mzee, mwanamume au mwanamke, sharti auawe.
14 Walimwapia Mwenyezi-Mungu kwa sauti kuu, wakapaza sauti zaidi, wakapiga tarumbeta na baragumu.
15 Watu wote wa Yuda walikuwa na furaha tele kwa kuwa walikuwa wameapa kwa moyo wote. Walikuwa wamemtafuta kwa dhati, wakampata. Naye Mwenyezi-Mungu akawapa amani pande zote.