18 Kuhani Yehoyada akaweka walinzi kulinda nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Hao walinzi walisimamiwa na makuhani na Walawi ambao Daudi aliwaweka katika huduma ya kutunza nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kutoa sadaka za kuteketezwa kwa Mwenyezi-Mungu kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, wakishangilia na kuimba kwa kufuata amri ya Daudi.
19 Aliweka mabawabu malangoni mwa nyumba ya Mwenyezi-Mungu ili asije akaingia mtu yeyote aliye najisi kwa namna moja au nyingine.
20 Aliwachukua makapteni wa jeshi, waheshimiwa, watawala wa watu, na wakazi wote; nao wakamsindikiza mfalme kutoka nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakapitia katika lango la juu mpaka ikulu. Kisha wakamkalisha mfalme kwenye kiti cha enzi.
21 Kwa hiyo wakazi wote walishangilia; na mji wote ulikuwa mtulivu baada ya Athalia kuuawa kwa upanga.