1 Ahazi alianza kutawala akiwa na umri wa miaka ishirini; alitawala kwa muda wa miaka kumi na sita huko Yerusalemu. Yeye, hakufuata mfano mzuri wa Daudi babu yake, bali alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu,
2 na kufuata mienendo ya wafalme wa Israeli. Isitoshe, alitengeneza hata sanamu za kusubu za Mabaali,
3 akafukiza ubani kwenye Bonde la mwana wa Hinomu na kuwateketeza wanawe kama tambiko, akiiga desturi za kuchukiza za watu ambao walifukuzwa na Mwenyezi-Mungu wakati Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini.
4 Alitoa tambiko na kufukiza ubani mahali pa kuabudia miungu mingine, vilimani na chini ya kila mti wenye majani mabichi.