4 Aliwaingiza makuhani na Walawi, kisha akawakusanya uani upande wa mashariki,
5 akawaambia, “Nisikieni enyi Walawi! Jitakaseni na itakaseni nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu. Toeni uchafu wote uliomo patakatifu.
6 Kwa maana babu zetu waliasi na kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Wamemwacha, wakageuzia mbali nyuso zao na kupawekea kisogo mahali aishipo Mwenyezi-Mungu.
7 Tena, waliifunga milango ya ukumbi, wakazizima taa, na hawajafukiza ubani wala kutoa tambiko za kuteketeza katika mahali patakatifu pa Mungu wa Israeli.
8 Kwa sababu hii, Mwenyezi-Mungu aliikasirikia sana Yuda na Yerusalemu, na yale aliyowatenda yamewashangaza na kuwaogofya watu wote, wakawazomea. Haya yote mmeyaona wenyewe kwa macho yenu.
9 Baba zetu waliuawa vitani, na wana wetu na binti zetu na wake zetu ni mateka kwa sababu hiihii.
10 Sasa, nimeamua kwa dhati kufanya agano na Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ili asitukasirikie zaidi.