7 Aliifunika nyumba yote kwa dhahabu: Boriti zake, vizingiti vyake, kuta zake na milango yake. Kutani palichongwa viumbe wenye mabawa.
8 Tena, alipatengeneza mahali patakatifu sana. Urefu wake ulikuwa mita 9, sawasawa na upana wake ambao pia ulikuwa mita 9. Alitumia zaidi ya tani 20 za dhahabu kukifunika chumba hicho.
9 Misumari aliyoitumia ilikuwa ya uzani wa gramu 570 za dhahabu. Pia alivifunika vyumba vyote vya ghorofani kwa dhahabu.
10 Alitengeneza sanamu mbili za viumbe wenye mabawa kwa mbao, akazifunika kwa dhahabu na kuziweka mahali patakatifu sana.
11 Kila kiumbe kilikuwa na mabawa mawili yenye urefu wa mita 4.4 jumla, mita 2.25 kila bawa. Bawa mojawapo liligusa ukuta upande mmoja wa chumba na la pili liligusana na la kiumbe wa pili.
12 Kadhalika bawa moja la kiumbe wa pili liligusa ukuta upande mwingine wa chumba na la pili likagusana na la kiumbe wa kwanza katikati ya chumba.
13 Urefu wa mabawa mawili ya viumbe hawa ni mita 4.5. Yalisimama sambamba, nyuso za viumbe wenye mabawa zikielekea ukumbini.