18 Aidha miongoni mwa kusanyiko hilo la watu, wengi wa wale waliotoka Efraimu, Manase, Isakari na Zebuluni, walikuwa wakiiadhimisha Pasaka kinyume cha maagizo. Hii ni kwa kuwa mfalme Hezekia aliwaombea akisema, “Mwenyezi-Mungu uliye mwema, msamehe yeyote yule
19 atakayekuomba kwa moyo wake wote wewe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zake, hata ingawa si msafi kulingana na sheria za utakaso.”
20 Mwenyezi-Mungu alikubali ombi la Hezekia, akawasamehe watu hao.
21 Waisraeli wote waliokuwa wamekusanyika mjini Yerusalemu waliiadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu kwa muda wa siku saba, wakiwa na furaha kubwa. Walawi na makuhani walimsifu Mwenyezi-Mungu kila siku, walimwimbia kwa nguvu zao zote.
22 Mfalme Hezekia aliwasifu na kuwatia moyo makuhani kwa kuwa waliendesha ibada kwa ujuzi mwingi.Baada ya kumaliza siku saba wakati ambao watu walikula, wakatoa sadaka za amani na kumtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao,
23 watu waliamua kwa kauli moja kuziendeleza sherehe kwa muda wa siku saba zaidi. Basi, wakaendelea kusherehekea kwa furaha kuu kwa muda wa siku saba zaidi.
24 Mfalme Hezekia wa Yuda aliwapa watu waliokusanyika jumla ya mafahali 1,000 na kondoo 7,000. Hali kadhalika, wakuu wakawapa mafahali 1,000 na kondoo 10,000. Idadi kubwa ya makuhani walijitakasa.