5 Kwa hiyo waliamua kutoa tangazo kote nchini Israeli, kutoka Beer-sheba hadi Dani, kwamba watu waje Yerusalemu kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Ulikuwa umepita muda mrefu kabla watu hawajaiadhimisha Pasaka kulingana na sheria zake.
6 Matarishi, kwa amri yake mfalme na maofisa wake, walipeleka barua kote nchini Israeli na Yuda. Barua hizo zilikuwa na ujumbe ufuatao:“Enyi watu wa Israeli mlionusurika baada ya mashambulizi ya wafalme wa Ashuru. Mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Israeli, ili naye apate kuwarudieni.
7 Msiwe kama babu zenu na ndugu zenu ambao hawakuwa waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, ambaye kama mnavyoona aliwaadhibu vikali.
8 Msiwe wakaidi kama babu zenu, ila mtiini Mwenyezi-Mungu. Njoni katika hekalu lake ambalo amelitakasa milele, mumwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ili asiwakasirikie.
9 Mkimrudia Mwenyezi-Mungu, wale ambao waliwateka ndugu zenu na watoto wenu, watawahurumia na kuwaacha warudi katika nchi hii. Kwa maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni mwenye rehema na huruma, naye atawapokea ikiwa mtamrudia.”
10 Basi, matarishi hao wakaenda toka mji mmoja hadi mwingine kote nchini Efraimu na Manase, wakafika hata Zebuluni. Lakini watu waliwacheka na kuwadhihaki.
11 Hata hivyo, watu wachache miongoni mwa makabila ya Asheri, Manase na Zebuluni, walijinyenyekesha wakaja Yerusalemu.